
Rapa kutoka Atlanta, Gunna, amethibitisha rasmi kwamba yeye na Offset wako kwenye maandalizi ya albamu ya pamoja. Taarifa hiyo ilikuja Septemba 22 jijini Los Angeles wakati wa onyesho maalum la Apple Music One Night Only, ambapo Gunna alichanganya mazungumzo ya kibinafsi na maonyesho ya moja kwa moja.
Akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu kilichoendeshwa na Ebro Darden, Gunna alieleza ni kwa nini ushirikiano wake na Offset unasikika wa kipekee:
“Kwanza kabisa, shout out kwa Offset, maana anatokea Atlanta pia. Na kila tunaposhirikiana ni natural, si kitu cha kulazimisha. Studio inakuwa fun, tunacheza na beats, Turbo naye anakuja, na tunashirikiana kama kawaida. Tunapeana nguvu, ndiyo maana muziki unakuwa na ile energy.”
Alipoulizwa moja kwa moja kuhusu uwezekano wa albamu ya pamoja, Gunna hakuwa na shaka:
“Ndiyo. Ipo njiani. Tumeipanga kwa utaratibu – yeye akatoa albamu yake, mimi nikatoa yangu. Mimi nilikuwa kwenye yake, yeye akawa kwenye yangu. Hizo zilikuwa kama chembechembe tu kuelekea kwenye mlo mkubwa unaokuja hivi karibuni.”
Gunna na Offset tayari wana historia ya kushirikiana kwenye nyimbo kadhaa, zikiwemo “Different Species,” “at my purest,” “prada dem,” na “Style Rare” (2024). Mashabiki wamesifia chemistry yao, na sasa albamu ya pamoja inaonekana kuwa hatua ya asili kufuatia mafanikio hayo.
Mbali na kutangaza mpango huo, Gunna aliwatumbuiza mashabiki akiwa na live band, akipiga nyimbo kutoka albamu yake The Last Wun – kazi yake ya mwisho chini ya YSL. Wimbo kama “cfwm,” “just say dat,” “forever be mine,” na “won’t stop” uliwasha moto ukumbini na kuonyesha upeo wa sanaa yake binafsi.