
Sean “Diddy” Combs amekuwa akiwafundisha wafungwa kozi maalum iitwayo Free Game With Diddy akiwa gerezani. Kozi hiyo ya wiki sita inafanyika katika Brooklyn Metropolitan Detention Center na inahusisha mpango wa masomo wa kurasa 15 unaolenga kuwapa washiriki ujuzi wa usimamizi wa biashara, ujasiriamali na maendeleo binafsi.
Kupitia barua waliyopeleka mahakamani, mawakili wa Diddy wamesisitiza kwamba mchango wake gerezani unapaswa kuzingatiwa wakati wa hukumu yake, wakipendekeza kifungo cha miezi 14 pekee baada ya yeye kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kusafirisha watu kwa madhumuni ya ukahaba mwezi Julai. Wamesema kwamba kozi hiyo imebadilisha maisha ya wafungwa wenzake, huku mmoja akiandika kuwa kupitia darasa hilo amepata kusudi na kitu cha kusubiri kila siku.
Hukumu ya Diddy imepangwa kusomwa Oktoba 3, 2025 huku upande wa mashtaka ukiendelea kushinikiza kifungo cha miezi 51 hadi 63. Aidha, mawakili wake wamewasilisha barua nyingi za kumtetea kutoka kwa familia na marafiki wake, ikiwemo Yung Miami aliyewahi kuwa mpenzi wake.