
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mpango wa kuandaa pambano la UFC katika viwanja vya Ikulu ya White House kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 250 ya uhuru wa Marekani mwaka ujao.
Akizungumza katika tamasha la “America 250” lililofanyika kwenye viwanja vya maonyesho ya jimbo la Iowa, Trump alisema:
“Kila moja ya maeneo yetu ya kitaifa ya kihistoria na vita vitakuwa na matukio maalum kuadhimisha America 250. Na tutakuwa na pambano la UFC — fikiria hilo — katika viwanja vya White House.”
Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, alithibitisha mpango huo na kusema kuwa rais “yuko makini kabisa” kuhusu wazo hilo. Msemaji wa UFC pia aliambia CNN kuwa wako kwenye majadiliano na Ikulu kuhusiana na tukio hilo, lakini hawakuwa na maelezo zaidi kwa sasa.Trump ana uhusiano wa muda mrefu na shirika la UFC pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wake, Dana White. Uhusiano wao ulianza tangu 2001, wakati White alipokuwa na changamoto za kupata ukumbi wa kuandaa pambano la UFC na Trump akaamua kulifanyia kwenye Trump Taj Mahal, Atlantic City.