Rc makonda aahidi kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameahidi kuhakikisha kuwa anawafanya vijana wa Mkoa wa Arusha kuweza kutambua na kutumia vipaji vyao katika kujiletea maendeleo, akiahidi kuwasaidia vitendea kazi na kuwatengea sehemu maalum za kukuza na kuoneshea vipaji vyao.


Mhe. Mkuu wa Mkoa Paul Makonda ametoa kauli hiyo leo jioni Aprili 28, 2024 kwenye Viunga vya Makao makuu ya Mkoa wa Arusha, alipokuwa akizungumza na Vijana wanaofanya maonesho ya kuendesha na kucheza na pikipiki maarufu Jijini Arusha kama Dede.

Mhe. Paul Makonda amekutana na kundi hilo mara baada ya kuona vipande vyao vya Video mitandaoni na kuahidi kuwatafutia eneo maalum kwaajili ya kufanyia maonesho yao akitambua kwamba kazi hiyo yaweza kuwa chanzo cha mapato kwao na sehemu ya kulipendezesha jiji la Arusha.

Mh. Mkuu wa Mkoa kadhalika amewaahidi vijana hao kuandaa mashindano ya kuendesha na kucheza na pikipiki ambapo ameahidi kuwa zawadi kwa Mshindi itakuwa Shilingi milioni kumi kwa mshindi wa kwanza, milioni saba kwa mshindi wa pili na mshindi wa tatu atajishindia shilingi Milioni tano za Kitanzania.


Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo pia kuwahimiza vijana wa Arusha kumtanguliza Mungu katika shughuli zao za kila siku, Kutambua na kunoa vipaji vyao pamoja na kuzingatia suala la nidhamu ili kuweza kufikia mafanikio na kuondokana na utegemezi.

Kwa upande wao baadhi ya Vijana hao wamemshukuru Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kuwatambua na kuamua kukutana nao na kusema kuwa hawakuwahi kuhisi kutambulika kiasi cha kuweza kuitwa na Mkuu wa Mkoa na hivyo wameahidi kuzingatia maelekezo ya Mhe. Mkuu wa Mkoa ili kuweza kufikia ndoto zao na kujikwamua na umaskini kwa kuifanya kazi yao kuwa kazi itakayowaingizia kipato.


Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa ameahidi pia kuwakutanisha vijana hao na viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini kesho Jumatatu Aprili 29, 2024 ili vijana hao waweze kutumika kwenye shamra shamra za kuelekea kilele cha siku ya wafanyakazi duniani, ambayo kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika Jijini Arusha katika viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Share: