
“Diddy” Combs tayari anaweka malengo ya kufanya comeback kubwa, hatua ambayo huenda ikamrudisha jukwaani kwenye Madison Square Garden.
Kwa mujibu wa wakili wake wa muda mrefu, Benjamin Brafman, nguli huyo wa muziki mwenye umri wa miaka 54 hafikirii tu kuhusu utetezi wake wa kisheria pia anapanga onyesho kubwa katika ukumbi huo maarufu wa jiji la New York mara tu atakapomaliza kifungo na kuachiwa huru.
“Atarudi Madison Square Garden,” alisema Brafman katika mahojiano ya hivi karibuni. “Na nilimwambia, nitakuwepo.”
Ingawa Diddy mwenyewe hajatoa kauli rasmi kuhusu mipango ya maonyesho yajayo, maneno ya Brafman yameibua ishara ya kwanza ya matarajio yake ya baada ya kifungo. Uwezekano wa kurejea kwenye jukwaa la Madison Square Garden lililoshuhudia baadhi ya nyakati muhimu zaidi katika taaluma yake, ikiwemo Bad Boy Family Reunion Tour unaashiria nia yake ya kurejesha nafasi yake kwenye taswira ya umma na tamaduni za muziki.
Hata hivyo, kurejea kwake bado ni jambo lisilo na uhakika. Wiki iliyopita, Diddy alinyimwa dhamana kwa mara ya pili, na kubaki kizuizini akisubiri hukumu yake iliyopangwa kutolewa Oktoba 3. Anakabiliwa na mashitaka kadhaa ya shirikisho kutokana na uchunguzi unaoendelea, na waendesha mashtaka bado hawajathibitisha kama kutakuwa na mashitaka mengine zaidi.
Tangu kukamatwa mapema mwaka huu, Diddy amekuwa kimya hadharani, lakini timu yake ya mawakili inasisitiza kuwa anazingatia kupona, kuungana tena na familia yake, na hatimaye kujenga upya maisha yake binafsi na kazi yake ya muziki.