Nyota wa muziki wa ‘pop’ justin timberlake amekamatwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa

Mwanamuziki nyota wa muziki wa ‘Pop’ Justin Timberlake amekamatwa mjini New York kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kushtakiwa rasmi jana Jumanne asubuhi kabla ya kuachiliwa bila dhamana.

Timberlake alikuwa Sag Harbour, kijiji tajiri huko Hamptons, mahali maarufu pa majira ya kiangazi kwa watu mashuhuri.

BBC inaripoti kuwa Timberlake alikamatwa baada ya saa sita usiku polisi walipomvuta kutoka kwenye gari lake la kijivu aina ya BMW kwa kuendesha gari licha ya ishara ya kusimama na kushindwa kukaa upande wa kulia wa barabara, kulingana na hati ya mashtaka.

Inasemekana maafisa walipomsimamisha, macho ya Timberlake yalikuwa “mekundu” na “harufu kali ya kinywaji chenye kileo ilikuwa ikitoka kwenye pumzi yake”, hati ya mashtaka ilisema.

Alikuwa akizungumza kwa mwenendo wa pole pole na alifanya vibaya katika majaribio ya kama yuko sawa kwa matumizi ya kileo, maafisa walisema huku hati ya mashtaka ikieleza kuwa alikataa kupumua kwenye kifaa cha kuthibitisha kama amelewa.

Share: