
Mtayarishaji wa muziki nchini Tanzania, anayefahamika kwa jina la Cukie Daddy (@thisiscukie), amewagusa wengi baada ya kusimulia hadithi ya kweli kuhusu chanzo cha ndoto yake ya muziki na jinsi msanii Harmonize amesaidia kuifanya kuwa hai.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Cukie Daddy alisimulia jinsi akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu aliota kwamba alikuwa anawatengenezea wimbo wasanii maarufu duniani, P-Square. Ndoto hiyo ilimsababishia kuchelewa kuamka, na alipofika shuleni, alikumbana na adhabu kali ya fimbo kutoka kwa mwalimu wa zamu mbele ya wanafunzi wote.
Licha ya kuchekwa na kudharauliwa na marafiki zake kwa sababu ya ndoto hiyo, Cukie Daddy anasema hakuwahi kukata tamaa wala kuacha kuipambania ndoto yake. Aliendelea kuamini katika kile alichokiona.
Miaka kadhaa baadaye, ndoto hiyo imekuja kuwa na sura ya ukweli. Katika hadithi yake hiyo, Cukie Daddy anamshukuru kwa dhati msanii na Mkurugenzi Mtendaji wa Konde Music Worldwide, @harmonize_tz, akisema amemsaidia kutimiza moja ya ndoto zake kubwa za utotoni. Hii inafuatia ushiriki wake katika kazi mpya ya Harmonize na Rude Boy, aliyekuwa memba wa Psquare.Hadithi ya Cukie Daddy ni dhihirisho tosha la safari ndefu ya wasanii wengi na inaonyesha nguvu ya ndoto, subira, na kutokata tamaa.