
Ye (zamani akijulikana kama Kanye West) anakabiliwa na mashitaka mapya ya unyanyasaji wa kingono na usafirishaji haramu kwa ajili ya ngono kutoka kwa mfanyakazi wake wa zamani.
Lauren Pisciotta, aliyekuwa msaidizi binafsi wa Ye kati ya mwaka 2021 hadi 2023, amewasilisha malalamiko mapya katika kesi yake dhidi ya rapa huyo, baada ya awali kumshutumu kwa unyanyasaji wa kingono na kumfuta kazi kimakosa. Kwa mujibu wa taarifa ya kwanza iliyoripotiwa na TMZ, malalamiko hayo mapya yanamhusisha Ye na mashitaka ya kushambulia kimwili na kingono, usafirishaji haramu kwa ajili ya ngono (sex trafficking), ufuatiliaji wa mtu (stalking), na kumzuia mtu kwa nguvu (false imprisonment), miongoni mwa mengine.
Malalamiko mapya yanadai kwamba “Ye alimfanyia Pisciotta matamshi ya matusi kuhusu mwili wake, alimtaka avae mavazi ya kubana, alimshika vibaya mara kwa mara, alilazimisha amshuhudie akifanya ngono na wanawake wengine, alimpelekea picha za ngono na kumtaka naye atume zake, na mara kwa mara alimtaka ajiunge naye kwenye ngono, jambo ambalo alikataa.”
Tuhuma za sex trafficking zinadai kuwa Ye alitoa “ahadi za uongo kuhusu kumsaidia kielimu au kikazi ili kumshawishi akubali mahusiano ya kingono,” na pia alitumia “nguvu na vitisho” kumlazimisha aingie kwenye mahusiano hayo.
Pisciotta aliwasilisha kesi ya kwanza mwaka 2024 kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, kufukuzwa kazi kimakosa na kuvunjiwa mkataba, kisha akaongeza madai mengine baadaye mwaka huo.