
Nicki Minaj amemshambulia Jay-Z kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akimtaka amlipe fedha anazodai ni stahiki yake kutokana na hisa alizokuwa nazo kwenye kampuni ya Tidal...
Katika madai yake ya hivi karibuni, Minaj amesema Jay-Z anamdai mamilioni ya dola kwa sababu ya asilimia 3 ya umiliki wa Tidal aliyopewa alipokuwa mmoja wa wasanii waanzilishi wa jukwaa hilo la muziki lililozinduliwa mwaka 2015. Wakati huo, hisa hizo zilikuwa na thamani ya dola milioni 56. Mwaka 2021, kampuni hiyo iliuzwa kwa dola milioni 302 kwa kampuni ya Square inayomilikiwa na Jack Dorsey. Minaj anasema kuwa aliambiwa angebaki na dola milioni moja tu kutoka kwenye mauzo hayo, badala ya kiasi cha takriban dola milioni 9 ambacho kingelingana na thamani ya asilimia 3 ya bei ya mauzo.
Kupitia ukurasa wake wa X, Minaj aliandika kuwa wamehesabu kuwa kiasi kinachodaiwa kwa sasa kiko kati ya dola milioni 100 hadi 200 na kumtaka Jay-Z awasiliane naye ili walimalize deni hilo analoliita “karmic debt.” Licha ya hayo, Minaj amesema bado anamuheshimu Jay-Z na kumuweka kwenye orodha ya wasanii wake wa juu zaidi. Pia alitaja kuwa iwapo atapokea fedha hizo, atazitumia kusaidia baadhi ya mashabiki wake kwa kulipa ada zao za shule kupitia taasisi yake ya misaada ya Student Of The Game.
Katika maelezo mengine, aliendelea kuishambulia kampuni ya Roc Nation na msanii wake Megan Thee Stallion, akimhusisha na kesi ya unyanyasaji wa kingono iliyowahi kuripotiwa dhidi ya Megan.