
Katika ulimwengu wa sasa wa muziki, Watoto na vijana wadogo ni soko linalopuuzwa, kwa mujibu wa Jermaine Dupri.
Akizungumza kwenye Podcast ya Joe Budden, huyu mtayarishaji nguli alisema kuwa kwa sasa hakuna nafasi katika tasnia ya muziki kwa wasanii wachanga kukua na kujengewa misingi ya mafanikio.
“Ni lini umeona mtu kama mimi anamchukua msanii kama Bow (Wow) na kumlea kwa miaka miwili hadi akawa vile alivyokuwa?” Dupri alihoji.
Dupri aliongeza kuwa binti yake mwenye umri wa miaka 14 hana msanii wa rika lake wa kumsikiliza:
“Yuko mitaani anasikiliza vitu ambavyo havimhusishi kabisa kwenye TikTok. Anacheza muziki ambao hatakiwi kucheza kwenye TikTok.”
Kwa mujibu wake, tasnia ya muziki imewasahau vijana wa kati ya miaka 12 hadi 16:
“Ni jukumu letu kuwaletea wasanii wanaowakilisha kundi hili, lakini hakuna mtu anayefanya hivyo. Siwezi kufanya kila kitu, lakini jukumu letu ni kuangalia kundi hili. Hivi sasa hakuna anayejali.”
Joe Budden naye alikubaliana, akisema kuna “pengO” kubwa, akitaja mfano wa dada yake mwenye umri wa miaka 11 ambaye ni shabiki mkubwa wa Tyler, The Creator. Dupri akajibu:
“Hakuna anayewaletea New Edition, hakuna anayewaletea Bow, hakuna anayewaletea Kris Kross. Hawajali.”
Kwa uzoefu wake wa zaidi ya miaka 30 kwenye muziki, Dupri anajua namna muziki wa vijana unaweza kubadilisha mchezo. Aliwahi kulea na kuongoza wasanii waliokuwa na mafanikio makubwa wakiwa bado vijana akiwemo Bow Wow, Kris Kross, Xscape na Da Brat.
Aidha, aliwahi kushirikiana na Queen Latifah kuunda kipindi cha uhalisia (The Rap Game), ambacho kilimsaidia Lattokuanza safari yake ya muziki.