
Katika kile kinachoweza kusemwa kama mfano wa hali ya juu wa maandalizi ya muziki kabla ya kifo, Ed Sheeran amefichua kuwa ameshajumuisha kwenye wosia wake maagizo ya kutolewa kwa albamu aliyipa jina la 'Eject' itakayotoka baada ya kufariki.
Akizungumza kwenye mahojiano na Zane Lowe kuhusu mipango yake ya mfululizo wa albamu mpya zinazofuatana na majina ya vitufe vya kicheza muziki, Sheeran alieleza kuwa baada ya Play (iliyotoka Septemba 12), ataendelea na Pause, Fast Forward, Rewind, na Stop. Lowe alipomuuliza kama Stop itakuwa albamu yake ya mwisho, Sheeran alijibu: “Kweli hapana. Itakuwa Stop na kisha Eject.”
Alipozua kicheko kwa Lowe, Sheeran alisisitiza: “Ipo kabisa kwenye wosia wangu! Na Cherry [Seaborn, mke wake] ndiye atakayechagua nyimbo. Imewekwa rasmi pale endapo nikifa kesho.”
Sheeran alifafanua kuwa anataka Eject iwe mkusanyiko wa nyimbo alizoandika “kuanzia nikiwa na miaka 18 hadi nitakapofariki — kisha zichaguliwe bora 10.” Akitoa mfano, alisema: “Fikiria kama Paul McCartney angefariki na kukawa na rekodi za Beatles za utotoni zikiunganishwa na kazi za mwisho za maisha yake — nyimbo bora kumi za taaluma yake yote. Wengi hawatapenda, lakini kwa mashabiki wangu wengi hilo litakuwa jambo la kipekee.”
Akaongeza kuwa mara nyingi albamu za posthumous huwa “hazijapangwa,” na yeye analenga kubadilisha hilo kwa kuweka mpangilio wa makini. Sheeran alisema atakuwa akizungumza na Cherry katika maisha yake yote kuhusu nyimbo anazozipenda, akisisitiza: “Sitaki nife kisha mtu aanze tu kuchanganya nyimbo na kuzitoa. Nataka iwe imepangwa.”