
Rapa maarufu anayejulikana kwa wimbo Am I The Drama? amethibitisha kupitia kipindi cha CBS Mornings kwamba yeye ni mjamzito na anatarajia mtoto wake wa nne, ambaye ni wa kwanza pamoja na nyota wa NFL, Stefon Diggs.
Msanii huyo mwenye asili ya Bronx alithibitisha habari hizo wakati wa mahojiano na Gayle King, ambaye hakuwa na hiyana kuuliza moja kwa moja kuhusu tetesi zilizokuwa zikisambaa mitandaoni. King alimwambia, “Kuna uvumi mitaani kwamba unatarajia mtoto, na ningependa kujua kama kuna chochote ungependa kushiriki kuhusu hilo.” Cardi alijibu, “Ndiyo, ni kweli. Natarajia mtoto na mpenzi wangu, Stefon Diggs.”
Cardi tayari ana watoto wawili, Kulture na Wave, aliowazaa na mume wake wa zamani Offset. Alisema anahisi nguvu na furaha kuingia tena katika maisha ya uzazi, akieleza kwamba yuko katika nafasi nzuri kihisia na kitaaluma. Aliongeza kuwa yeye na Diggs wanasaidiana sana na kushirikiana kwa kuwa wote wako kileleni katika taaluma zao, na wana mtazamo wa kutotulia bali kuendelea kupanda viwango zaidi.
Msanii huyo pia alionyesha jinsi Diggs anavyomfanya ajihisi salama na kujiamini. Akitania, alisema kuwa ukubwa wa mchezaji huyo unampa hisia za ulinzi wa kimwili na kisaikolojia, kiasi kwamba anahisi anaweza kutawala dunia.
Ingawa uvumi ulikuwa ukizunguka kwa muda, Cardi alisema alitaka kutoa taarifa hiyo kwa wakati wake mwenyewe, akisisitiza kwamba hakuwa akificha, bali alikuwa akisubiri kukamilisha baadhi ya mikataba kwanza. Kwa ucheshi aliongeza, “Sasa nimezungumzia, basi hakikisheni mnanunua albamu yangu ili nipate hela za kununua nepi na Pampers.”
Kwa mshangao wa wengi, Cardi alifichua kwamba hata wazazi wake hawakuwa bado wamejulishwa, na aliahidi kuwaambia kabla ya mahojiano hayo kurushwa. Alieleza kuwa yeye na Diggs walitamani kuongeza familia zao, na licha ya ushauri wa watu kumwambia ajiburudishe zaidi, walijikuta wakibeba ujauzito ambao sasa unawaletea furaha kubwa.
Mbali na habari za ujauzito, Cardi yupo mbioni kutoa albamu yake ya pili iliyosubiriwa kwa miaka saba, na amepanga kuanza ziara ya muziki mwezi Februari, wiki chache tu baada ya kujifungua.