Basata yatoa neno mvutano kati ya marioo na barnaba juu ya tuzo za (tma)

Kutokana na mvutano unaoendelea kwenye mtandao wa Instagram kati ya wanamuziki Elias Barnabas, ‘Barnaba’ na Omary Ally, ‘Marioo’, kuhusu Tuzo za Muziki Tanzania kutotenda haki kipengele cha albamu bora ya mwaka 2023 Basata imesema malalamiko hayo bado hayajawafikia.

Kumekuwa na majibizano kwenye mitandao ya kijamii baada ya Marioo kuwatuhumu waandaaji wa tuzo za Muziki Tanzania (TMA) kuwa hawatendi haki kwani tuzo ya album bora iliyotolewa 2023, alistahili kushinda yeye na badala yake ikaenda kwa Barnaba.

Mkurugenzi wa Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa ‘Basata’, Edward Buganga akizungumza leo Mei 21, 2024 amesema utolewaji wa tuzo hizo huzingatia taratibu na kufuata vigezo.

“Hayo ni maoni ya watu, maoni na utaratibu ni vitu viwili tofauti, lakini inapotokea tuzo kuna taratibu zinafuatwa za kuwatunuku watu, kuna vigezo maalumu lazima vinafuatwa kimoja baada ya kingine,” amesema Buganga.

Ikumbukwe mvutano huo ulianza baada ya Marioo kulalamikia albamu yake ya “The Kid You Know” kutoshinda tuzo na badala yake ikashinda “Love Sounds Different” ya Barnaba kama Albamu Bora Mwaka 2022, ambayo tuzo yake ilitoka 2023.

Kutokana na mvutano huo, Buganga amesema hadi sasa bado wasanii hao hawajafikisha malalamiko yoyote Basata.

“Suala hilo halijafika kwetu, likitufikia kuna utaratibu wa kufanyia kazi, mlalamikaji na mlalamikiwa, tuna wataalamu wa kutosha wa kushughulikia suala hilo, kuna timu ya wanasheria, likifika tutashughulika nalo.

“Lengo letu ni kufanya kazi vizuri na wasanii wote wana haki sawa na Basata ni nyumbani kwao,” amesema.

Share: