
Rapa kutoka Harlem, A$AP Rocky, ameeleza kutoridhishwa kwake na jinsi ugomvi wa kimuziki kati ya Drake na Kendrick Lamar ulivyoishia, hasa hatua ya Drake kumpeleka Universal Music Group (UMG) mahakamani kwa madai ya kashfa na unyanyasaji kufuatia wimbo “Not Like Us.”
Akizungumza na jarida la ELLE (Septemba 23), Rocky alisema:
“Sichukii ugomvi huu, ila sikupenda ulivyogeuka hadi Drake kufungua kesi. Hiyo ni sehemu gani ya mchezo? Hiyo ni nini sasa? Lakini, mwisho wa siku, si biashara yangu.”
Hata hivyo, alikiri kwamba mzozo huo ulioibua mashambulizi ya nyimbo kati ya Drake na Kendrick ulikuwa “mzuri na wenye afya kwa Hip Hop.”
Mwezi Aprili 2024, A$AP Rocky alishiriki kwenye mashambulizi hayo kupitia wimbo wa Future na Metro Boomin “Show of Hands,” ambapo alimrushia Drake dongo kuhusu uhusiano wake na Sophie Brussaux, mama wa mtoto wa Drake. Mistari hiyo ilileta mjadala mkubwa, huku Drake akijibu kupitia “Family Matters.”
Pamoja na hayo, Rocky hakusukuma mbele zaidi mashambulizi yake. Alieleza:
“Ilikuwa vita kati ya Kendrick na Drake, si Drake dhidi ya kila mtu. Ndiyo maana niliamua kurudi nyuma.”
Mwaka jana, akizungumza na Billboard, mwanzilishi wa A$AP Mob alisema aliamua kujitenga na malumbano hayo kwa sababu ana mambo makubwa zaidi ya kushughulika nayo:
“Kuna mambo makubwa mitaani. Watu wanapoteza maisha kila siku, hivyo ugomvi wa muziki haukuwa jambo kubwa sana kwangu.”
Kwa namna ya kejeli, Drake alipokuwa anaimba “Family Matters,” alitabiri kwamba Rocky angebeba mtoto mwingine kabla ya kutoa albamu yake mpya “Don’t Be Dumb.” Katika mahojiano yake mapya, Rocky alikubali kuwa maisha ya familia yamekuwa sehemu ya safari yake:
“Hatukupanga kupata watoto zaidi, lakini yakitokea lazima ukubaliane nayo na uendelee mbele.”