Serikali ya marekani imefuta baadhi ya leseni zilizowaruhusu watengenezaji chip nchini marekani kuuza bidhaa hizo china

Tangu mwaka wa 2019, Marekani imezuia mauzo ya teknolojia, kama vile chip za kompyuta, kwa Huawei

Serikali ya Marekani imesema imefuta baadhi ya leseni zilizowaruhusu watengenezaji chip nchini Marekani kusafirisha bidhaa fulani kwa kampuni kubwa ya teknolojia ya China Huawei.

Idara ya Biashara haikubainisha ni vibali vipi vilivyofutwa lakini hatua hiyo imekuja baada ya Huawei kutoa kompyuta inayoweza kutumia AI (akili mnemba) inayoendeshwa na chip iliyoundwa na Intel.

Tangu mwaka wa 2019, Marekani imezuia mauzo ya teknolojia, kama vile chip za kompyuta, kwa Huawei, ikibainisha sababu kuwa uhusiano na jeshi la China.

"Tumebatilisha leseni fulani za mauzo ya nje kwa Huawei," Idara ya Biashara ilisema katika taarifa Jumanne, lakini haikutoa maelezo ya vibali vilivyoondolewa.

Baadhi ya wabunge wa Marekani walikuwa wamekosoa utawala wa Rais Joe Biden kufuatia uzinduzi wa mwezi uliopita wa kompyuta ya mkononi ya Huawei ya MateBook X Pro.

Huawei imeathiriwa sana na vikwazo vya biashara vya Marekani lakini hivi karibuni ilionekana kurudi tena.

Kampuni ya China imefurahia ufufuo hasa baada ya kuzinduliwa kwa simu mahiri ya Mate 60 Pro mwezi Agosti.

Marekani imeweka vikwazo kwa makampuni kadhaa ya teknolojia ya China katika miaka ya hivi karibuni, huku mvutano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani ukizidi.

Mapema mwezi huu Rais Biden alitia saini sheria ambayo inaweza kupiga marufuku programu ya video ya TikTok nchini humo isipokuwa iwe inauzwa na kampuni mama ya China. TikTok iliwasilisha kesi Jumanne kuzuia sheria hiyo.

Beijing imelaani hatua za Washington dhidi ya kampuni zake, na kuzitaja kama 'unyanyasaji wa kiuchumi'.

Share: