META :  VITUO VYA "AI" VYA JENGWA KWA MABILIONI YA DOLA

Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa Meta, Mark Zuckerberg, ametangaza mpango mkubwa wa kuwekeza mamia ya mabilioni ya dola katika ujenzi wa vituo vikubwa vya data kwa ajili ya maendeleo ya teknolojia ya akili bandia (AI) nchini Marekani.

Kupitia chapisho kwenye jukwaa lake la kijamii, Threads, Zuckerberg alieleza kuwa Meta inajenga vikundi vya AI vyenye nguvu ya “multi-gigawatt”, ikiwa ni sehemu ya azma ya kampuni hiyo kuongoza katika kile kinachoitwa “superintelligence” – akili bandia inayoweza kuwazidi binadamu katika uwezo wa kufikiri.


Mradi wa kwanza, unaoitwa Prometheus, unatarajiwa kuanza kazi mwaka 2026 huko New Albany, Ohio, huku kituo kingine kikubwa, Hyperion, kikijengwa Louisiana na kinatarajiwa kukamilika ifikapo 2030, kikifikia nguvu ya hadi gigawatt tano.


Zuckerberg alisema baadhi ya maeneo haya yatakuwa makubwa kiasi cha kulingana na ukubwa wa Manhattan (takriban kilomita za mraba 59), akieleza kuwa majina ya vituo hivyo yanaendana na ukubwa na athari zao.


Meta, ambayo ilipata zaidi ya dola bilioni 160 mwaka 2024 kupitia matangazo ya mtandaoni, sasa inaelekeza rasilimali kubwa katika maendeleo ya AI, ikiwa na lengo la kuwa kinara duniani katika miundombinu ya teknolojia hiyo.


Mchambuzi wa masuala ya AI kutoka kampuni ya Cambrian AI Research, Karl Freund, anasema: “Ni wazi kuwa Zuckerberg analenga kufikia kilele cha teknolojia ya AI kwa kutumia uwezo mkubwa wa kifedha,” na kuongeza kuwa Meta inaajiri vipaji bora ambavyo vitatumia “vifaa vya kisasa zaidi vya AI duniani.”


Baada ya tangazo hilo, thamani ya hisa za Meta ilipanda kwa asilimia 1, huku shirika la habari la Reuters likiripoti kuwa hisa za kampuni hiyo zimepanda kwa zaidi ya asilimia 20 tangu mwanzo wa mwaka.


Hata hivyo, miradi hii mikubwa imeibua wasiwasi kuhusu athari za mazingira. Vituo vya data vinavyotumia AI hutumia kiwango kikubwa cha umeme na maji. Utafiti mmoja unakadiria kuwa vituo hivyo vitatumia hadi lita trilioni 1.7 za maji kote duniani ifikapo mwaka 2027, huku ombi moja la AI — kama vile mazungumzo na ChatGPT — likitumia maji sawa na yaliyomo katika chupa ndogo ya duka.

Share: