Upasuaji huo umeshirikisha timu ya watalaamu kutoka Muhimbili na madaktari bingwa wa taya na uso (5)
Hospitali ya Taifa Muhimbili, leo kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji wa kutoa mfupa kwenye ubavu na kutengeneza kiungio (joint) cha taya la chini na fuvu ili kumtengenezea mgonjwa taya jipya la kulia lililoathiriwa na uvimbe.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso na Taya Dkt Arnold Augustino amesema mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye nyonga pande zote mbili ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu ili kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalumu na kutengeneza sehemu ya taya iliyoharibika na ugonjwa.
Amesema, mara baada ya upasuaji huu mgonjwa huyo anategemea kuendelea kula na kutafuna kama kawaida kwani atawekewa meno bandia kwenye mfupa wa taya aliotengenezewa
Dkt Augustini ameongeza kuwa mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji aina tatu tofauti kwa wakati mmoja, wa kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe ambapo umechukua saa saba.
Upasuaji huo umeshirikisha timu ya watalaamu kutoka Muhimbili na madaktari bingwa wa taya na uso (5) wataalamu usingizi na ganzi (2) manesi wa upasuaji (3) na wataalamu wengine waliokuwepo ni pamoja madaktari wanaosomea ubingwa wa kupasua mataya na uso (3)