Makamu wa rais ataka wigo zaidi uwekezaji viwanda vya kimkakati

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazalishaji wa viwandani kuongeza wigo wa uwekezaji katika viwanda mbalimbali vya kimkakati vinavyozalisha bidhaa za kati hususan vile vinavyozalisha ajira kwa wingi, kuchochea ubunifu, tija na vyenye uhusiano mkubwa na sekta nyingine.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya utoaji Tuzo za Rais za Mwaka kwa Wazalishaji Bora iliyofanyika katika Ukumbi wa Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam. Amesema kwa sasa viwanda vinafanya vizuri kiasi katika kuzalisha bidhaa za walaji, vinywaji, vyakula, bidhaa za ujenzi hususan saruji, nondo, marumaru na mabati hata hivyo viwanda hivyo bado vinategemea sehemu kubwa ya malighafi zake kutoka nje.

 

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI) kubainisha sekta, sekta ndogo na viwanda zinavyokua haraka ambavyo tayari zimefanikiwa kujipenyeza katika masoko ya kikanda na kimataifa ili kubaini nini kinachohitajika kushughulikiwa na sekta binafsi, Serikali au kwa ubia ili kuviwezesha viwanda hivyo viweze kuongeza tija, uzalishaji na mauzo kama sehemu ya mkakati wa kufikia ndoto za Watanzania 2050.

 

Aidha amewasihi wenye viwanda kubuni mikakati ya kujihami dhidi ya athari zinazotokana na dhoruba katika uchumi wa dunia pamoja na kuchukua hatua zaidi kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za uzalishaji wao ikiwa ni pamoja na urejelezaji wa taka ngumu kama plastiki.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wazalishaji wa bidhaa za viwandani na Sekta Binafsi kwa ujumla kutumia nguvukazi kubwa ya vijana iliyopo pamoja na kuanza kuwapatia vijana fursa zaidi za mafunzo ya vitendo kazini ili kuongeza ujuzi wao na kuwadhamini. Ameielekeza CTI kuanza kuratibu na kuwatumia wazalishaji wa viwandani waliofanikiwa katika kutoa mafunzo kwa wanafunzi vyuoni.

Makamu wa Rais amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha viwanda vinakuwa katika mazingira wezeshi yanayoweza kuchochea ufanisi na ushindani katika masoko. Ametaja hatua hizo ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi zinazojumuisha kuimarisha usafiri wa anga na reli sambamba na upanuzi na uboreshaji wa utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kurahisisha upakiaji na utoaji wa mizigo kwa haraka.

Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea na jitihada katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo Nishati kama vile kufikia hatua za mwisho kukamilisha mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere –JNHPP (99.21%), ujenzi wa kongani za viwanda, ikiwemo Kongani ya Viwanda ya Kwala, Kongani ya Kisasa ya Viwanda (Modern Industrial Park) ya Mlandizi, na Ujenzi wa Miundombinu ya Msingi katika Kongani ya Viwanda – TAMCO, Kibaha pamoja na Wizara ya viwanda na biashara ikikamilisha Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika. Lengo ni kuongeza wigo wa soko kwa wazalishaji wa bidhaa za viwandani na Wafanyabiashara kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda nchini Paul Makanza ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto mbalimbali zilizowakabili wazalishaji wa viwandani kama vile ukosefu wa nishati ya uhakika ya umeme, mfumo rafiki wa kodi, kuimarishwa kwa upatikanaji wa fedha za kigeni, kuimarika kwa thamani ya shilingi na udhibiti wa mfumuko wa bei nchini.


Share: