Kampuni ya Sony imezindua Gari lake la kwanza la umeme aina ya Afeela 1, ikiwa ni matokeo ya ushirikiano wake na Kampuni ya Honda wakiunda ushirikiano wa Sony Honda Mobility ambapo rasmi wamezindua Gari hilo katika Maonyesho ya Watumiaji wa Elektroniki (CES) 2025 Mjini Las Vegas, Marekani.
Afeela 1 ni Gari lenye milango minne ambalo limebuniwa kwa teknolojia ya kisasa likiwa na uwezo wa kusafiri hadi kilomita 480 kwa chaji moja ambapo bei ya Gari hili inaanzia dola 89,900 (takriban shilingi za Kitanzania 222 milioni) huku toleo la juu zaidi likigharimu dola 102,900 (takriban shilingi 257 milioni).
Gari hili lina muundo wa kisasa wenye teknolojia za hali ya juu kama kamera na sensa 40 zinazoboresha usalama na kukusanya data kutoka mazingira yake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Sony Honda Mobility Yasuhide Mizuno Afeela 1 limeundwa kwa ajili ya kuendana na mahitaji ya enzi hizi za Magari yanayojiendesha yenyewe likiwa na lengo la kuboresha safari kwa usalama na starehe.
Kwa sasa uzalishaji wa Gari hili unatarajiwa kufanyika katika kiwanda cha Ohio, Marekani na usambazaji utaanza mwaka 2026 pia Gari hili limepangwa kuuzwa katika masoko ya Marekani na Japani huku mipango ya kuingia soko la Ulaya ikitarajiwa mwishoni mwa muongo huu.