Dk. Doto Biteko ametoa maelekezo tanesco kuangalia namna ya kuwawezesha wateja kupiga simu bila kulipia gharama

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa maelekezo kwa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuangalia namna ya kuwawezesha wateja kupiga simu bila kulipia gharama.

 Akizungumza Dar es Salaam leo Aprili 4, 2024, baada ya kutembelea kituo hicho kilichopo Ubungo, Dk Biteko amesema Watanzania wengi licha ya kulipia Luku kila mwezi, bado ni maskini na wanatakiwa kuendelea kuhudumiwa na Serikali.

“Lazima muangalie utaratibu wa wateja wetu wanaopiga simu kulipa hela, mimi siamini kwa nini tuendelee kumtoza mteja wetu anayelipia Luku kila mwezi, lakini likitokea tukio moja tunamtoza hela lazima tutafute mazingira ya mteja kupiga simu ahudumiwe bila gharama yoyote,” amesema.

Dk Biteko aliyeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio, amesema jambo hilo litasaidia wateja kuwa karibu na shirika na hata ikitokea amepatwa na changamoto, mathalani ya kuungua nyumba yake atasaidiwa haraka.

“Mfano mtu nyumba yake inaungua moto na kwenye simu hana hela atafanyaje, si mteja anasubiri kifo, tufikirie anaweka umeme, fedha anayotumia kununua umeme basi tulichokipata kwake tukirudishe kwa sababu hata yeye kupiga simu ni kwa sababu hatujatekeleza wajibu wetu,” amesema.

Share: