Watanzania jitokezeni kutoa maoni  miswada ya sheria ya uchaguzi na vyama vya siasa - dkt. biteko

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita katika Sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemus Maganga ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika kutoa maoni kuhusu muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 ili kuunga mkono jitihada za Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kujenga Tanzania iliyo bora zaidi katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita katika Sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemus Maganga ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

“Mhe. Rais amepeleka miswada hii bungeni iliyosomwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge na tangazo limeshatoka la kuwaomba wananchi kwenda kutoa maoni yao bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari 2024 kuhusu marekebisho ya sheria hizi, niwaombe watanzania, nendeni mkatoe maoni yenu ili kujenga Tanzania iliyo bora kuliko kubaki nyuma kulalamika.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzania wa vyama, dini na makabila mbalimbali, vilevile anasikiliza malalamiko ya makundi mbalimbali na kuyafanyia kazi akitolea mfano suala la kuruhusu Vyama vyote vya Siasa nchini kufanya mikutano ya hadhara ili kueleza sera zao na kwamba nia ya Rais ni kujenga mshikamano na umoja nchini.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi walio bora na kwamba watu wasigawanyike na kufarakana sababu ya uchaguzi, bali waungane katika uchaguzi huo kwa kuzungumza yale yanayowaunganisha kama vile barabara, maji, umeme na wasiruhusu mtu kupandikiza chuki katikati yao.

Katika salam zake za mwaka 2024, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuhusu watanzania kupendana, kuthaminiana, kuvumiliana, kusameheana, kuwa na shukrani, kusaidiana na kumfanya mtu mwingine afurahi, huku lengo likiwa ni kujiletea maendeleo kwa pamoja.

Kuhusu hali ya upatikanaji umeme wilayani Mbogwe, Dkt. Biteko amesema kuwa, itaendelea kuimarika kwani imejengwa njia mpya ya umeme ambayo itapeleka umeme wilayani humo kutokea kituo cha Nyakanazi, pia itajengwa njia nyingine ambayo itapeleka umeme Mbogwe kutokea Kahama na pia kitajengwa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wilayani humo kama ambavyo ujenzi wa vituo hivyo utakavyofanyika katika wilaya nyingine nchini.

Share: