RC Tanga awaongoza wananchi kupiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, leo ameongoza zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa katika kituo cha Raskazone Swimming Club, jijini Tanga.

Akizungumza baada ya kupiga kura, Dkt. Batilda amewataka wananchi wa mkoa wa Tanga kujitokeza kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. 

Alisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki katika kuamua mustakabali wa maendeleo ya mitaa yao kwa kuwachagua viongozi bora.


“Hii ni haki yetu ya msingi kama wananchi, Ninatoa wito kwa kila mmoja kujitokeza mapema kupiga kura na kisha kurudi nyumbani kwa utulivu kusubiri matokeo” alisema Balozi Dkt. Batilda.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unahesabika kuwa msingi wa maendeleo ya jamii, ambapo wananchi hupata nafasi ya moja kwa moja kushiriki katika maamuzi yanayowagusa. 

Katika mkoa wa Tanga, wananchi wameonekana kuhamasika kufika vituoni mapema, huku hali ya amani ikiripotiwa kote.

Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa baada ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika.

Share: