Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amemtaka Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Bw. Tundu Lissu kwenda mahakamani, ikiwa ana ushahidi wa kutosha kuwa Mkuu huyo wa Mkoa alihusika kwenye shambulizi lake la kutaka kuuwawa Septemba 17, 2017.
Makonda ametoa kauli hiyo leo Novemba 17, 2024 kwenye kituo cha Kimataifa cha AICC Jijini Arusha mbele ya wanahabari na wananchi wa Mkoa wa Arusha wakati akitoa tathimini ya utendaji kazi wa miezi sita tangu kuteuliwa kwake na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Katika maelezo yake, Mhe. Makonda ameeleza kuwa Septemba 17, 2017 wakati huo akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam alikuwa na tukio la usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa matibabu bure kwa wakazi wa Jiji la Dar Es salaam kwenye viwanja vya Mnazi mmoja, na hakuwa Dodoma kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na Tundu Lissu na baadhi ya wanasiasa.