Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ameahidi kutunza Upendo na heshima aliyopatiwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kuwa wageni wote kutoka nchi nane za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanakuwa salama kwa kipindi chote watakachokuwa Arusha kusherehekea Miaka 25 ya jumuiya hiyo
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo usiku wa leo Novemba 28, 2024 wakati wa Mkesha wa kuelekea maadhimisho ya Miaka 25 ya EAC, akiwashukuru wenyeji na wageni wote kutoka nje ya nchi kwa kujitokeza kwao kwa wingi kwenye Usiku wa kukaribisha sherehe hizo zinazofanyika Mkoani Arusha ikiwa ni ishara ya Upendo kwa Rais Samia ambaye ni muandaaji wa Mkesha huo.
Mhe. Makonda pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia na serikali yake kwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoelekezwa Mkoani Arusha, akiwataka wahudhuriaji wa Mkesha huo kutumia vyema fursa ya kukutana pamoja raia wa mataifa nane tofauti kutoka barani Afrika wakiwa na Mawaziri zaidi ya 30 wa nchi hizo ili waweze kunufaishana kiuchumi na kijamii.
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo amempongeza Mhe. Makonda kwa ubunifu wake na utekelezaji mzuri wa maagizo ya serikali hasa kwa namna alivyoshirikiana na Sekretarieti ya EAC kwenye maandalizi ya sherehe za miaka 25 ya Jumuiya hiyo ya Kikanda.