
Rais William Ruto ametangaza rasmi uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali ombi lililopinga mchakato huo.
Katika Tangazo la Serikali nambari 9269 la Julai 10, 2025, Rais Ruto amemteua Erastus Edung Ethekon kuwa Mwenyekiti mpya wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita.
Katika tangazo tofauti, nambari 9270, pia la tarehe 10 Julai 2025, Rais amewateua Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallahkuwa makamishna wa IEBC kwa kipindi sawa cha miaka sita.
Hatua hii imekuja baada ya Mahakama Kuu kubaini kuwa uteuzi wenyewe ulikuwa halali, lakini notisi ya awali ya gazeti la serikali ilikiuka agizo la mahakama, hivyo ikatupiliwa mbali na kutakiwa kuchapishwa upya.
Kupitia matangazo mapya yaliyotolewa, mwenyekiti na makamishna hao sasa wanatarajiwa kula kiapo mbele ya Jaji Mkuu ili kuanza rasmi kazi zao katika tume.