mwitikio wa wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ni mkubwa na mawakala wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo
Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameonesha kuridhishwa na zoezi la Uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaoendelea katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara ambapo hadi kufikia jana Wapiga Kura 1,613 wamejitokeza.
Wajumbe hao wa Tume, Mhe. Jaji Asina Omar, Mhe. Jaji wa Rufaa Mwanaisha Kwariko na Mhe. Magdalena Rwebangira wametembelea vituo vya uboreshaji katika Kata ya Ikoma na kushuhudia ufanisi wa zoezi hilo.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, Jaji Asina Omar amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ni mkubwa na mawakala wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuwabaini wananchi wasio na sifa za kuandikishwa kuwa Wapiga Kura.
Jaji Asina amesema, muda unaotumika kuandikisha au kuboresha taarifa za Mpiga Kura unazidi kuwa mfupi na kuimarika kwa huduma vituoni hivyo kuleta ufanisi zaidi siku hadi siku na kuonesha uwezo wa vifaa vinavyotumika.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira amesema ameridhishwa namna zoezi linavyofanyika hivyo lengo la zoezi hilo la kufanyia majaribio vifaa vya uboreshaji pamoja na mifumo ya uboreshaji wa Daftari linatimia kwani changamoto zinabainika na kutatuliwa mapema.
Akitoa taarifa ya siku nne za uboreshaji huo wa majaribio katika Kata ya Ikoma, Mkurugenzi wa Idaya ya Usimamizi wa Uchaguzi, Ndg. Grayson Orcado kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema, zoezi hilo linakwenbda vizuri na kwa ufanisi mkubwa kwani hadi sasa wananchi 1,613 wamejitokeza vituoni ambapo kati ya hao 1,356 wamejiandikisha kuwa wapiga kura na wapiga kura 257 wameboresha taarifa zao huku hakuna walioondolewa katika Daftari.
Orcado amesema, mawakala wa vyama wanaonesha ushirikiano wa hali ya juu hasa katika changamoto za utambuzi wa wakazi wa maeneo yao kwa kuzingatia kuwa Kata ya Ikoma inamwingiliano wa raia wanchi jirani.
Kwa mujibu wa mawakala wa vyama waliokuwepo katika kituo cha kujiandikisha wapiga kura cha Shule ya Msingi Nyamasanda, walieleza kuwabaini raia 8 wakigeni kutoka nchi jirani ambao walikiri kuwa si watanzania na hivyo Mwandishi Msaidizi hakuweza kuwaandikisha kuwa wapiga kura.
Wakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Silvanus Owan’ge aliyepo katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji Kata ya Ikoma amesema, wanarisdhishwa namna zoezi hilo lilivyo la uwazi na kupongeza Tume kwa namna inavyofanya kazi kwa kushirikiana nao.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendesha zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara na Kata ya Ng’ambo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.