Kesi hiyo imesitishwa huku mzozo huo ukielekea katika mahakama kuu nchini humo
Kesi ya kihistoria, ambayo inaweza kuathiri hatima ya kisheria na kisiasa ya Donald Trump na kufafanua wigo wa mamlaka ya urais, itafikishwa mbele ya majaji tisa wa Mahakama ya Juu ya Marekani siku ya Alhamisi.
Mawakili wa Bw Trump na Wakili Maalum Jack Smith watajibu hoja zao katika kesi ya iwapo marais wa zamani hawana kinga ya kushtakiwa kwa makosa ya jinai kwa hatua wanazochukua wakiwa madarakani.
Bw Smith alimshtaki rais huyo wa zamani mwaka jana kwa madai ya kujaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa 2020. Lakini Bw Trump alisema hawezi kushtakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Marekani.
Kesi hiyo imesitishwa huku mzozo huo ukielekea katika mahakama kuu nchini humo.
Kesi hiyo tayari ni ya kihistoria: Bw Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani kushtakiwa kwa uhalifu wa serikali kuu.
Na uamuzi wa Mahakama ya Juu, ambao hautatolewa hadi Juni, utakuwa pia muhimu.
Ikiwa mahakama itaamua Bw Trump anaweza kufunguliwa mashtaka, basi kesi hiyo itasonga mbele, lakini huenda itaanza tena mwishoni mwa majira ya kiangazi mapema zaidi, katikati mwa msimu wa uchaguzi wa urais. Iwapo itaamua kuwa ana kinga, Bw Trump anaweza kushuhudia kesi nyingine za uhalifu dhidi yake zikitupiliwa mbali.
Bw Smith aliishinikiza mahakama kufanya uamuzi mnamo Desemba, lakini ilikataa.
"Richard Nixon alisema kuwa watu wa Marekani wanastahili kujua iwapo rais wao ni mhalifu," alisema Kermit Roosevelt, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania. "Mahakama ya Juu haionekani kukubaliana na hilo. Wako sawa kwa kuzuia hili kuamuliwa kabla ya uchaguzi."