Aidha, tume hiyo imesema kwamba uchaguzi uliofanywa na maafisa wa tume hiyo uliangazia kuvunjwa kwa sheria za kupiga kura na vile vile visa vya utovu wa usalama ambavyo vilishuhudiwa katika baadhi ya maeneo.
Tume huru ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imefutilia mbali uchaguzi uliofanyika katika majimbo ya kadhaa nchini humo kufuatia kile imesema ni kupatikana na ushahidi wa kutosha kwamba sheria za uchaguzi zilivunjwa.
Taarifa ya hatua hiyo, ilichapishwa Ijumaa, huku CENI ikisema kwamba ripoti ya uchunguzi uliofanyika ulionyesha kwamba katika uchaguzi wa ubunge na udiwani baadhi ya wagombea viti hivyo walishiriki katika udanganyifu na hivyo uchaguzi wao umefutiliwa mbali.
Wabunge wateule, takriban 80 wameathirika katika majimbo ya Kwilu,Yokama, Ubangi,na Equateur.
Aidha, tume hiyo imesema kwamba uchaguzi uliofanywa na maafisa wa tume hiyo uliangazia kuvunjwa kwa sheria za kupiga kura na vile vile visa vya utovu wa usalama ambavyo vilishuhudiwa katika baadhi ya maeneo.
"Jopo la uchunguzi la CENI linaendelea kupokea ripoti za uharibifu wa mali ya umma na vifaa vya kupigia kura, madai ya watu binafsi kupata vifaa vya kielktroniki vya kupigia kura, na vile vile kushambuliwa kwa wafanyikazi wa tume ya CENI." Alisema Patricia Nyesa, afisa mkuu wa CENI.
Tume hiyo imesema pia inawachunguza wafanyikazi wao ambao wanadaiwa kushirikiana katika kuvunja sheria za uchaguzi za DRC.
Huku CENI ikiendeleza uchunguzi wake, hatima ya walioathirika sasa iko mikononi mwa vitengo vya usalama na idara ya mahakama ambapo wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka mbalimbali.
Hayo yakijiri,mahakama ya kikatiba nchini humo inaendelea kusikisa kesi ya kupinga uchaguzi huo wa DRC wa Desemba 20 2023, iliwasilishwa na mgombea huru wa Urais Theodore Ngoy, aliyelalamikia hali ilivyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Aidha inatarajiwa pia uongozi wake kwenye kesi iliyowasilishwa na kanisa nchini humo kupata ufafanuzi wa kikatiba kuhusu kuongezwa kwa muda wa kupiga kura , utatolewa katika siku chache zijazo.