Dkt. biteko ataka umoja wa vijana ccm kushikamana

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 8 Januari, 2024 amefungua Kongamano la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kongamano hilo ambalo limefanyika katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi limeambatana na matembezi ya vijana nchi nzima kuhamasisha umuhimu wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi Maendeleo.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ni silaha ya Chama katika uchaguzi na kupeleka maendeleo kwa wananchi na kwamba CCM inaona fahari na heshima kubwa kuwa na vijana kama wao, “hata uchaguzi ukija tuna uhakika nguvu kubwa ya ushindi ipo, nawapongeza kwa kuweka rekodi na kuthibitisha kuwa mpo imara kwani rekodi hii bado haijawekwa na chama chochote kile.”

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Zanzibar, amesema kuwa, kuna mabadiliko makubwa na miradi inayofunguliwa ni mingi na kwamba, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi anafanya kazi kubwa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifanya katika kuwapelekea maendeleo wananchi hasa walio maskini ili kuinua hali zao za kiuchumi na kuweka miundo mbinu wezeshi ya kiuchumi.

Kutokana na juhudi hizo zinazofanywa na Viongozi Wakuu wa nchi katika kuwaletea wananchi maendeleo, ameitaka UVCCM kuhakikisha wanawasaidia viongozi hao katika kuyasemea mazuri wanayoyafanya tena bila kificho.

Katika utendaji kazi wa UVCCM, Dkt. Biteko ametoa angalizo kuwa, kwa sasa kuna wasomi wengi nchini na mitandao yenye kuunganisha watu wengi lakini suala hilo lisiwafanye waogope kutekeleza majukumu yao kwa kuwa watakosolewa kwani kukosea kupo katika safari ya mafanikio.

Share: