Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimekanusha vikali madai ya kuwa kwenye mazungumzo na Chama cha Kisiasa ambacho hawakukitaja Jina, ili kuweza kugaiwa baadhi ya majimbo na nafasi za madaraka katika muundo wa serikali.
Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa CHADEMA Bw. John Mrema amewaambia wanahabari kuwa Chadema katika vikao vyake vyote rasmi haijawahi kujadili, kutoa ama kupokea mapendekezo yoyote ya kitu kinachoitwa "Serikali ya Nusu mkate" kama ambavyo linapotoshwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii na kuzusha taharuki ya wanachama wake kutaka kujua na kupata ufafanuzi wa jambo hilo.
Aidha Chadema imesema haijawahi kuiacha ajenda yake ya kutaka Katiba mpya na madai ya mfumo huru wa uchaguzi katika utekelezaji wa programu zake kwasababu yoyote ile kama inavyotaka kuaminishwa kwa jamii.
Katika hatua nyingine Chadema imesema ipo mstari wa mbele kupambana na ufisadi, ubadhirifu na rushwa, na kutaka ushahidi dhidi ya tuhuma za uwepo wa fedha chafu na rushwa ndani ya Chama hicho wakati huu wa uchaguzi wa ndani.
"Kama chama kikiletewa ushahidi au vielelezo vya tuhuma hizo kutoka kwa mtu yeyoye tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo ya Chama dhidi ya rushwa ya mwaka 2012.Hivyo tunamualika mtu yeyote mwenye ushahidi unaojitosheleza kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu bhasi awasiliane na ofisi ya Karibh Mkuu au Katibu yeyote wa Kanda." Imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Bw. John Mrema